
Wanawake katika mkoa wa Kigoma magharibi mwa Tanzania wanalazimika kuyatoroka makaazi yao kutokana na hofu ya visa vya ubakaji vinavyodaiwa kutekelezwa na kundi linalojulikana kama 'teleza'.
Mashirika ya kiraia yanaeleza kuwa kumeshuhudiwa visa 43 vinavyojulikana vya wanawake kubakwa tangu 2016 mpaka April mwaka huu.
Hatahivyo yanashutumu kwamba hatua madhubuti hazijachukuliwa kukabiliana na visa hivyo.
Polisi nchini inaeleza kwamba washukiwa kadhaa wamekamatwa.
Lakini je 'teleza' ni kina nani na ni kwanini wanawabaka wanawake?
'Teleza' kama wanavyofahamika, inaarifiwa ni kundi la vijana wanaodaiwa kutokuwa na shughuli.
Jina hilo limetokana na mtindo wao maarufu wanaotumia wa kujipaka mafuta machafu meusi katika miili yao kuepuka kutambulika na pia kuwasidia kushopoka kwa kuteleza wanapojaribu kukamatwa.
Vijana hao inaarifiwa wamekuwa wakiwahangaisha wanawake katika eneo hilo kwa muda sasa na kwa mujibu wa mashirika yasio ya serikali Tanzania likiwemo la kutetea haki za wanawake -TAMASHA - kumeshuhudiwa visa zaidi ya arobaini tangu mwishoni mwa mwaka 2015 mpaka Aprili mwaka 2019 vya wanawake waliobakwa na kundi hilo la 'Teleza'.
Wanawake wanaolengwa ni pamoja na wajane, wale wasioishi na waume zao, wasichana wadogo na hata wazee.

Mashirika hayo yamekuwa yakishinikiza hatua ichukuliwe katika kukabiliana na tatizo hilo wakati maafisa wa utawala wakieleza kwamba ni visa vya uchache tu.
Shirika hilo la kiraia miongoni mwa mengine yanadai kwamba licha ya maafisa kujaribu kuingilia kati kuitatua hali, bado ubakaji wa wanawake unashuhudiwa na takwimu kamili haijulikana ya ukubwa wa tatizo lenyewe.
Wanawake wanaishi kwa uoga:
Baadhi ya wanawake mkoani kigoma, magharibi mwa Tanzania, wanalazimika kuhama makazi yao ama kulala kwa kurundikana kwenye chumba kimoja ili kukwepa wabakaji wanaotumia mtindo wa ubakaji maarufu kama 'teleza'.
Inaarifiwa kwamba wengi wa wanawake hao wanahofia kujitokeza wazi kuzungumzia masaibu hayo kutokana uoga wa kutambuliwa kutishiwa maisha na pia unyanyapaa uliopo katika jamii kwa waathiriwa.
Jeshi la Polisi linasema limekuwa likifanya msako dhidi ya wahalifu hao na tayari limewakamata baadhi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo vya ubakaji.
Katika maeneo ya Mwanga Kigoma wanawake wameiambia BBC kwamba 'Teleza sio wa kitoto...'
Hii ni baada ya kundi hilo kudaiwa kuwaendea zaidi ya mara tatu wanawake hao sehemu walipokuwa wanaishi.
Baadhi yao sasa wameamua kuyahama makaazi yao na wengine kulazimika kurundikana chini kwenye chumba kimoja kama wanavyofanya wengine katika kulikwepa kundi la Teleza.
Aisha, ni mmoja wa waathiriwa wa teleza na alivamiwa mara 2. Kwa sasa anajipanga kuhama mkoa huo kabisa.
Ukimuangalia amekata tamaa, ana makovu usoni,….miguuni… teleza walimjeruhi kwa kisu wakijaribu kumbaka.
'Familia yote tuko watu 7, tunalala chumba kimoja, tunaweka godoro chini tunalala. Kama akiingia akitukata sote, basi, sasa unfanyaje'.
'Na mpango wa kuhama na sio kuhama tu, nataka kuhama Kigoma nzima, najipanga tu mambo yakiwa sawa nitaondoka', anasema Aisha.
Vijana sasa wameanzisha doria kuimarisha ulinzi katika eneo hilo kuwalinda wanawake.
Ali Ruango ni mmoja wa vijana katika kikundi cha ulinzi wa kujitolea katika eneo hilo.
'Tunapiga doria za usiku kila siku, hatahivyo tunaogopa kutembea na silaha, silaha yao (teleza) kubwa ni kisu na panga, kuna wakati unaweza kushika panga alafu ukakutana na mtu akajua wewe ndiye Teleza'.
Wanaharakati wa wanawake Kigoma, wanaona kuhama ama kurundikana chumba kimoja kwa wanawake sio suluhu ya kudumu, wakigusia pia hofu yao kuhusu afya za wanawake wanaobakwa, na uchumi wao wanapohama na kuacha shughuli zao.
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, hivi karibuni limewatia nguvuni, watuhumiwa 9 wa teleza akiwemo anayedaiwa kinara wao, na kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya ya Kigoma mjini, zoezi la kutokomeza kundi hilo la teleza ni endelevu.
chanzo: bbc
Comments
Post a Comment