
Samatta ambaye ni kinara wa ufungaji wa klabu ya Genk ambao ni mabingwa wa Ligi ya Ubelgiji, anawaniwa na klabu kadhaa za England.
Akizungumza na runinga ya Azam TV, mshambuliaji huyo amesema yupo tayari kuchukua nafasi ya Romelu Lukaku wa Man United endapo atapata nafasi.
Lukaku amekuwa na wakati mgumu Old Trafford msimu uliopita na amekuwa akihusishwa na mipango ya kutaka kuhamia klabu ya Inter Milan.
Alipoulizwa na Azam TV endapo anaweza kuvaa viatu vya Lukaku Samatta alijibu: "Kwanini nishindwe? Naweza kuvaa. Mafanikio yanaweza yasiwe kama niliyopata Genk, lakini naweza kucheza, sababu mpira ni uleule. Tayari nipo Ulaya na najua nini natakiwa kufanya kwenye ligi za Ulaya. Itakuwa ni klabu kubwa na presha itaongezeka mara dufu, yaweza kuwa vigumu kuzoea mwanzoni lakini mwisho nitazowea."

Streka huyo mwenye miaka 26, ameifungia Genk magoli 23 na kumaliza kama mshambuliaji bora wa ligi. Pia ameifunga magoli 9 kwenye michuano ya ligi ya Europa.
Jina la Samatta limekuwa likiimbwa na mashabiki wa Genk, na wamekuwa wakimuomba mshambuliaji huyo kusalia klabuni hapo kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya.
"Hawa jamaa (Genk) hawajacheza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2011 enzi za akina (Kevin) De Bruyne, najua wanataka nicheze msimu ujao lakini Ligi Kuu ya England ina heshima yake...ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana kulinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, Ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani. Yaani kwa vitu vingi iko mbali," amesema Samtta.
Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.
Kabla ya kujiunga na Mazembe alikuwa akiichezea klabu ya Simba ya Tanzania.
chanzo: bbc
Comments
Post a Comment