NA MWANDISHI WETU
BAADA ya kurejea katika michuano ya kimataifa, beki wa Yanga, Andrew Vincent, ‘Dante’, amewapa habari njema mashabiki wa timu hiyo, akisema hawataichezea bahati ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga iliyoshika nafasi pili Ligi Kuu Tanzania Bara, imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuongeza idadi ya timu kutoka mbili hadi nne za Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa.
Uamuzi wa Caf kuongeza timu, unatokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12 zilizofanya vizuri katika michuano ya shirikisho hilo kuanzia msimu wa 2014/15 hadi sasa, ikijikusanyia pointi 18, tatu zikitokana na mafanikio ya Simba 2018/19 kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
Mbali ya Yanga, timu nyingine itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa ni Simba ambao ni wababe wa Ligi Kuu Bara, huku Azam ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu nyingine ya Tanzania itakayoshiriki michuano ya CAF ni KMC walioshika nafasi ya nne Bara, ambao watakipiga Kombe la Shirikisho kwa kuwa tayari Azam walishakata tiketi hiyo kupitia ubingwa wao wa ASFC 2018/19.
Kutokana na hilo, Dante alisema wao ni wazoefu wa michuano hiyo, kwani wameshiriki mara nyingi, lakini hawakuwa na bahati ya kufika mbele zaidi kama walivyofanya wapinzani wao wa jadi Simba.
“Tumejua tulikosea wapi huko nyuma na sasa tumepata nafasi ya kushiriki michuano hii tena, tutakuwa makini kuhakikisha tunafanya vizuri na kufika mbali zaidi,” alisema.
Dante alisema anaamini kocha wao atafanya marekebisho makubwa katika kikosi chao ili kucheza soka la ushindani.
Comments
Post a Comment