Serikali ya Tanzania imewarai raia wake kuwa watulivu kufuatia matamshi ya mbunge mmoja wa Kenya aliyewatishia wageni wanaoishi nchini humo ikiwemo raia wa Tanzania.
Kanda ya video iliomuonyesha mbunge wa Starehe nchini Kenya Charles Kanyi maarufu Jaguar akitishia kuwafukuza raia wa kigeni aliowatuhumu kuchukua biashara za Wakenya ilisambaa katika mitandao ya kijamii nchini humo siku ya Jumanne.
''Wakenya ni sharti wafanye biashara zao bila kushindana na watu kutoka mataifa mengine. Raia wa Pakistan wametawala biashara za kuuza magari nchini humu, Watanzania na Waganda wanatawala katika masoko yetu. Tunasema imetosha iwapo hawatarajeshwa nyumbani katika saa 24 tutawashika na kuwapiga na hatuogopi mtu yeyote'', alinukuliwa akisema.
Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, matamshi hayo hayakupokelewa vyema katika bunge la Jamhuri ya Tanzania, huku Mbunge wa Rufiji kupitia chama cha CCM Mohammed Mchengerwa akimtaka spika kutoa uongozi kuhusu umuhimu wa serikali ya taifa hilo kutoa taarifa kuhusu usalama wa raia wa Tanzania ambao wanaishi na kufanya kazi pamoja na biashara nchini Kenya.
Gazeti hilo lilimnukuu spika wa bunge hilo akiagiza serikali kutoa taarifa kuhusiana na hilo huku waziri mkuu Kassim Majaliwa akisema kuwa serikali ililichukua swala hilo na umuhimu mkubwa na kumtaka balozi wa Kenya nchini Tanzania kujieleza.
''Tulimuita mjumbe wa Kenya nchini Tanzania. Pia tulizungumza na mjumbe wa Tanzania nchini Kenya. Mwanadiplomasia huyo wa Kenya alisema kuwa lilikuwa tamshi la kibinafsi ambalo halikuhusishwa na msimamo wa serikali ya Kenya. Aliahidi kwamba serikali itamuhoji mbunge huyo kuelezea kile alichomaanisha katika matamshi yake'', alisema Majaliwa.
Huku akiwataka raia wa Tanzania kuwa watulivu kufuatia ombi la mwanadiplomasia huyo wa Kenya , bwana Majaliwa alisema kuwa taarifa hiyo pia ilikosolewa na wabunge wa bunge la Afrika mashariki ambao walikuwa wakifanya kikao mjini Arusha.
''Sisi kama Watanzania tuendeleeni kuishi na amani na Wakenya hatuna matatizo nao'', alisema.
Kulingana na gazeti hilo bwana Majaliwa aliwataka raia wa Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi pamoja na Sudan Kusini kutokubali kutoa matamshi ambayo yanakiuka makubaliano ya umoja wa Afrika mashariki.
Tayari serikali ya Kenya kupitia msemaji wake kanali mstaafu Cyrus Oguna imetoa taarifa yake ikisema kuwa matamshi ya mbunge huyo ni ya kibinafsi na kwamba sio msimamo wa serikali ya Kenya.
'' Tungependa kusema kuwa huo sio msimamo wa serikali ya Kenya na tunashutumu matamshi hayo yaliotolewa katika kanda hiyo ya video. Matamshi hayo hayafai katika ulimwengu wa sasa'', alisema Oguna.
''Wakenya ni wapenda amani ambao kwa miaka mingi wameishi na raia wengine wa kigeni bila tatipo lolote. Hii ni thamani ambayo tunajivunia kama taifa na ni lazima tuendelea nayo'', ilisema taarifa hiyo iliotiwa saini na msemaji huyo wa serikali.
Taarifa hiyo imesema kuwa serikali ya Kenya inachukulia yaliomo katika kanda hiyo na umuhimu mkubwa na tayari imeanza kuchukua hatua kali za kisheria.
Aidha serikali ya Kenya imewahakikishia raia wote wa kigeni na wale walio na hamu ya kutaka kuwekeza nchini humo kuhusu usalama wao pamoja na mali yao.
Awali gazeti la The Citizen nchini Tanzania liliandika kwamba wabunge walitoa matamshi dhidi ya mbunge huyo wa Kenya huku wakisubiri serikali kutoa msimamo wake rasmi na wakati mmoja spika wa bunge Job Ndugai alisema kuwa matamshi hayo ya Jaguar hayawezi kuwa msimamo wa serikali ya Kenya. ''Tusilichukulie hili kuwa sawa''.
''Iwapo kuna taifa katika jangwa la sahara barani Afrika ambalo raia wake wanapatikana kwa wingi katika kila taifa na zaidi , basi taifa hilo ni Kenya'', alisema kiongozi wa upinzani bungeni Freeman Mbowe.
Karibu kila mbunge ambaye alijadili suala hilo alimkosoa Jaguar, akisema matamshi yake hayafai na kwamba serikali ya Kenya ilihitajika kutoa taarifa ya kumshutumu.
source: bbc
Comments
Post a Comment