Zahera kuwasilisha mapendekezo ya usajili kwa uongozi Yanga
Baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, uongozi wa Yanga utakutana na kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera ambapo pamoja na mambo mengine, Zahera atawasilisha mapendekezo yake ya usajili, imefahamika
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema kikao hicho ni cha pili kufanyika tangu uongozi mpya uingie madarakani
Amesema kikao cha kwanza kilikuwa cha Kamati ya Utendaji ambacho kiliweka maazimio mawili, moja; kuhakikisha Yanga inashinda michezo mitatu iliyobaki na la pili linahusu usajili
"Kikao chetu kilikuwa na agenda mbili, moja ni usajili ambao tutakutana na Zahera baada ya kumaliza mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting na nyingine kumaliza ligi kwa heshima," amesema
"Tulivyopewa uongozi, timu ilikuwa inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo tumeweka mikakati kushinda mechi zote tatu zilizobaki na kujua hatima yetu huko mbele"
Katika kikao hicho inaelezwa Zahera atawasilisha majina ya wachezaji ambao ametaka waendelee kubaki Yanga ili kuanza mchakato wa kuhuisha mikataba kwa wale ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu
Zahera pia atawasilisha majina ya wachezaji wapya anaotaka kuwasajili
Jumamosi ya wiki hii May 18 Yanga imeandaa tukio la futari na chakula cha jioni litakalofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam ambapo kwenye tukio hilo itafanyika Harambee ya kuichangia Yanga
Wageni mbalimbali wanatarajiwa kualikwa katika Harambee hiyo wakiwemo wabunge, mashirika mbalimbali ya Serikali na binafsi, taasisi za dini na wadau wote wenye mapenzi na Yanga
Aidha siku hiyo Kamati ya Hamasa itakabidhi kwa uongozi kiasi cha fedha ambazo zimekusanywa tangu kuanzishwa kwa kampeni ya kuichangia Yanga
KWA TAARIFA ZA MICHEZO KILA SIKU
PAKUA APP YA MIKOGO HAPA
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.mikogo.blog
Comments
Post a Comment