Msimu huu Yanga imemaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia alama 86
Ni msimu ambao ulikuwa na changamoto nyingi hasa kwa wachezaji, hata hivyo walijitolea, kuipigania Yanga kuhakikisha inapata mafanikio
Wachezaji wengi waliopewa nafasi na kocha Mwinyi Zahera walifanya vizuri
Hawa hapa wachezaji walion'gara zaidi;
Heritier Makambo
Wakati akisajiliwa na Yanga, Makambo hakuwa akifahamika na mashabiki wengi wa soka nchini
Lakini amemaliza msimu akiwa amefunga mabao 17 katika ligi kuu ya Tanzania Bara
Ameifungia Yanga mabao 23 kutoka michezo takribani 42 aliyoitumikia Yanga katika michuano yote
Ni mmoja wa wachezaji walion'gara katika kikosi cha Yanga msimu uliomalizika akiwa amecheza mechi nyingi pia
Ni bahati mbaya kwa Yanga kumpoteza mshambuliaji wake huyu tegemeo ambaye anaelekea Guinea kujiunga na Horoya AC
Lakini pia ni bahati nzuri kwani Yanga imejipatia faida kutokana na mauzo yake, fedha ambazo zitatumika kuboresha kikosi
Ibrahim Ajib
Ajib alikuwa na msimu mzuri sana kwenye kikosi cha Yanga hasa kwenye duru ya kwanza ligi kuu ya Tanzania Bara
Amefunga mabao sita na kutoa pasi 17 za mabao, yeye ndiye kinara wa kutoa pasi za mabao msimu uliomalizika
Licha ya kuwa mchezaji aliyekuwa na 'dharura' nyingi zilizomfanya akose michezo mingi, lakini ufanisi wake katika michezo aliyocheza uliisaidia sana Yanga
Kutokana na umuhimu wake kocha Mwinyi Zahera alimteua kuwa nahodha wa kikosi chake akichukua majukumu ya Kelvin Yondani
Baada ya kukataa kujiunga na TP Mazembe, bado haijafahamika kama ataongeza mkataba Yanga au ataelekea Simba, timu aliyotoka misimu miwili iliyopita
Abdallah Shaibu 'Ninja'
Ninja ndiye beki aliyecheza mechi nyingi zaidi msimu huu. Umuhimu wake ulionekana pale walipokosekana mkongwe Kelvin Yondani na Andrew Vicent
Msimu huu Shaibu aliboresha kiwango chake mara dufu na halikuwa jambo la kushangaza kwa yeye kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa umri chini ya miaka 23 na akateuliwa kuwa nahodha wa timu hiyo
Kelvin Yondani
Yondani amekuwa 'bosi' wa safu ya ulinzi ya Yanga kwa miaka mingi. Uzoefu na umahiri wake unaisaidia Yanga kuendelea kufanya vizuri.
Papi Tshishimbi
Alianza msimu kwa kusuasua kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara
Hata hivyo tangu aliporejea katika kikosi cha kwanza, Tshishimbi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia sana Yanga
Aidha, licha ya kubadilishiwa majukumu kutoka kiungo mkabaji na kuwa msaidizi wa mshambuliaji (namba 10) Tshishimbi aliendelea kuwa bora akifanikiwa kufunga mabao manne
Paulo Godfrey 'Boxer'
Wengi wamemshangaa kocha Emmenuel Amunike kutomjumuisha kinda huyu kwenye kikosi cha timu ya Taifa kinachokwenda kushiriki michuano ya AFCON 2019 nchini Misri
Paulo ni mmoja wa wachezaji walion'gara sio Yanga tu, hapaswi kukosekana kwenye kikosi bora cha ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu
Nadhani ukizungumzia beki wa bora wa kulia kwa sasa hapa Tanzania lazima utamtaja Boxer aliyepandisha kikosi cha kwanza na Zahera
Feisal Salum 'Fei Toto'
Fei Toto anaweza kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi kwenye kikosi cha Yanga msimu huu
Kiungo huyo kinda mwenye umri wa miaka 20 alikuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya Yanga
Ni kadi za njano pekee ambazo zilimfanya akose mechi za Yanga
Ameifungia Yanga mabao manne kwenye ligi
Mrisho Ngasa
Mkongwe huyu usajili wake ulibezwa sana, lakini kazi aliyoifanya kwenye kikosi cha Yanga ni kubwa
Ni winga aliyejihakikishia nafasi kwenye kikosi cha Zahera ambacho kilikuwa na mabadiliko na mara kwa mara
Ngasa ndio winga pekee ambaye alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha kwanza kwenye mechi nyingi licha ya mabadiliko hayo ya mara kwa mara
Hakuna shaka, mkongwe huyo ataendelea kubaki Jangwani, kwani uzoefu wake utaweza kuisaidia Yanga msimu ujao
Miongoni mwa wachezaji hawa na wengine ambao hawakutajwa, je unadhani nani anastahili kuwa mchezaji bora wa Yanga msimu huu?
Comments
Post a Comment