Klabu ya Waasland Beveren inayoshiriki Ligi Kuu Daraja la Kwanza kule Ubelgiji ambayo ilimalizika juzi usiku kwa Genk ya Mbwana Samatta kubeba taji, inahitaji huduma ya Makambo na kwamba imeweka mzigo mrefu kuliko ule wa Horoya.
MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kuanza kutabasamu sasa. Hawana sababu ya kuendelea kukunja sura kama zamani, kwani mabosi wapya wa klabu hiyo wameingia na gia kubwa na kuhakikisha Yanga inarejesha heshima yake na kunukia harufu ya fedha.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania wananukia harufu ya ankara, kwani habari mpya ni juu ya kuuzwa kwa straika wao namba moja, Heritier Makambo ikiwa imeleta neema mpya baada ya klabu moja ya Ulaya kuingia vitani kumhitaji mshambuliaji huyo.
Wakati Makambo akivumishwa kujiunga na Horoya AC ya Guinea iliyomfanyia vipimo vya afya wiki iliyopita, kisha kuingia nao mkataba wa awali sasa biashara inakaribia kugeuka.
Klabu ya Waasland Beveren inayoshiriki Ligi Kuu Daraja la Kwanza kule Ubelgiji ambayo ilimalizika juzi usiku kwa Genk ya Mbwana Samatta kubeba taji, inahitaji huduma ya Makambo na kwamba imeweka mzigo mrefu kuliko ule wa Horoya.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinasema, Bareven imeweka mzigo mrefu kushinda ule wa Horoya yaani unaingia mara mbili na kubaki ili wampate Makambo.
Usishangae unaambiwa klabu hiyo ilipotajiwa Makambo anatoka Tanzania tu alikozaliwa mshambuliaji anayesumbua kiatika ligi yao, Mbwana Samatta mwenyekiti wa klabu hiyo, Dirk Huyck, aliamua kuzuia dili la mshambuliaji Msenegal akitaka aletewe Makambo.
Beveren imewaambia Yanga waachane na habari ya Dola 100,000 (Sh 230 milioni) na kwamba wao wako tayari kuweka mezani bila kupungua Dola 200,000 (Sh 460 milioni).
Tayari Yanga imeshajulishwa kila kitu juu ya ofa hiyo na sasa mabosi wakubwa wa timu hiyo chini ya uongozi wa Dk Mshindo Msolla na makamu wake, Fredrick Mwakalebela wanapiga hesabu wakiangalia dili lipi litawafaa, japo tayari wameshalainika na fedha za Wabelgiji hao.
Kuonyesha jamaa hawataki mchezo Mwanaspoti linafahamu mwakilishi wa klabu hiyo ameshakatiwa tiketi ya ndege na Huyck, kuja nchini ambapo katika barua yao wamekubali kutoa tiketi mbili za ndege kwa Makambo na bosi mmoja wa Yanga kuungana naye katika umalizwaji wa dili.
Endapo dili hilo litakamilika litakuwa ni faida kubwa kwa Yanga ambayo ilimsajili Makambo kama mchezaji huru ikitumia Dola 15,000 ( Sh 33.4 milioni) kwa mkataba wa miaka miwili ambapo sasa mwisho wa msimu huu atakuwa amebakiza mkataba mwaka mmoja taslimu.
Yanga inahitaji fedha hizo katika kuwavutia washambuliaji watatu ambao wanawahitaji ambao kama Makambo atauzwa watavutika kirahisi kuja kujiunga na timu hiyo wakiona ni kama wanatua njia panda ya Ulaya.
Ofa hiyo ya Makambo pia itawaamsha Horoya AC ambayo imeshaingia mkataba wa awali na Makambo kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha zaidi katika kumsajili Mkongomani huyo aliyefunga jumla ya mabao 20 akifunga 16 ya Ligi Kuu na manne ya Kombe la FA. Hata hivyo, mkataba wa Mambo na Horoya hautaizuia kwa vyovyote Yanga kufanya biashara na timu nyingine.
Tayari Horoya ilishaweka bayana kumlipa Makambo kiasi cha Dola 5,000 (Sh 11 milioni) kwa mwezi kama dili hilo lingekamilika na kumsajili mwisho wa msimu.
Yanga katika kujiandaa na maisha bila Makambo tayari imeshawakusanya washambuliaji kadhaa huku ikiachana huduma ya straika Mzimbabwe, Rodrick Mutuma ambaye klabu yake ya FC Lupopo imeweka ngumu kumuachia kujiunga na Yanga msimu ujao.
Comments
Post a Comment