
MOMBASA. OFISA Mtendaji Mkuu wa Bandari FC, Edward Oduor amekanusha tetesi zinazosambaa mjini hapa na kule Tanzania kuwa, kipa Farouk Shikhalo atasajiliwa na klabu ya Yanga msimu ujao wa 2019-2020.
Oduor alisema uvumi wa Shikhalo kusajiliwa na Yanga inachipuka kwa mara ya pili kwani, mwishoni mwa msimu uliopita, zilitambaa hasa huko jijini Dar es Salaam.
“Shikhalo angali yuko na mkataba na Bandari kwa miaka miwili ijayo na wanaozungumza juu ya kusajiliwa na Yanga, wanapoteza muda kwani, hilo halitawezekana,” alisema.
Pia, alikanusha uvumi kwamba, nahodha wa timu hiyo Felly Mulumba naye ataondoka kwenda Kusini mwa Afrika kujiunga na klabu moja. “Hakuna ukweli wa uvumi huo kwani, Mulumba angali na mkataba nasi wa mwaka mmoja,” akasema.
Akithibitisha hilo, bosi huyo akizungumza kwa simu akiwa Nairobi wakisubiri kwenda Machakos kwa mechi yao ya SportPesa Shield dhidi ya SS Assad FC ya Ukunda hapo kesho, Oduor alisema Mulumba yuko kwenye kikosi hicho japo hatacheza mechi hiyo.
“Ningependa kufahamisha wenye kuongea juu ya wachezaji wetu kuhama, ni kuwa wote wana mikataba na Bandari. Wenye kutaka kusubiri wasubiri, lakini wachezaji wote watabakia kuichezea timu msimu ujao,” alisema.
Comments
Post a Comment