FEI TOTO KUTIMKIA BURNLEY!

Juu ya tetesi za kutakiwa Burnley iliyopo Ligi Kuu ya England, Kambi alisema ni mapema kwa sasa kuzungumzia hilo.


HUENDA taarifa hii ikawa nzuri kwa mashabiki wa Yanga. Hii ni baada ya kiungo fundi wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuamua kuvunja ukimya na kuzima tetesi za kusepa kwake Jangwani kipindi hiki ambacho Straika, Heritier Makambo akiwa njia kutimka zake.

Ipo hivi. Kwa wiki nzima sasa, kumekuwa na taarifa Fei Toto alikuwa mbioni kutimka zake nje ya nchi kucheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa ikiwamo Burnley ya Uingereza, lakini yeye na meneja wake wamefichua ukweli wa mambo ulivyo.

Inaelezwa uwepo wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 inayotarajiwa kuanza mwezi ujao pale Misri, ambako Tanzanioa imepangwa na Senegal ya Sadio Mane, Algeria ya Riyaz Mahrez na Kenya ya Victor Wanyama imemzuia kusepa Yanga.

Meneja wa Fei Toto aliyesajiliwa na Yanga kimafia msimu huu kutoka JKU, Zubeir Kambi alisema kwa sasa mchezaji wake hawezi kutimka Jangwani kwani akili zote zipo kwenye ushiriki wa fainali za Afcon akiwa na kikosi cha Taifa Stars cha Emmanuel Amunike.

Kambi alifichua ni kweli zipo klabu kadhaa zinazomtaka mteja wake, baada ya kutuma video za mchezaji wake sehemu mbalimbali ili kuona kama anaweza kupata mialiko na amefanikiwa kwa asilimia kubwa, ila waansubiri Afcon iipite ndipo wajue cha kufanya.

“Kweli kuna timu zinamtaka kwa ajili ya majaribio na nyingine zinamhitaji moja kwa moja, hivyo lolote litakalotaka na klabu yake ya Yanga inafahamu, ila kwa sasa tunakuwa wapole kwani akili zake zipo Afcon 2019,” alisema Kambi.

Juu ya tetesi za kutakiwa Burnley iliyopo Ligi Kuu ya England, Kambi alisema ni mapema kwa sasa kuzungumzia hilo.

“Ndugu yangu watu watasema hivi na vile, halafu mbona huko mbali sana, kitu muhimu jua kwamba zipo ofa nzuri mezani na wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi na bahati nzuri ofa zote ni nzuri kwa kijana kwenda kuendeleza maisha yake kisoka,” alisema Kambi anayewasimamia nyota kadhaa wakiwamo Hassan Dilunga, Mohammed Issa, Ally Ng’anzi na Charles Masenga na aliwahi kusimamia dili la Yohana Mkomola alipotakiwa kukipiga huko Etoile du Sahel ya Tunisia, japokuwa lilikwama na sasa yupo Ukraine akikipiga na klabu ya Arsenal Kiev.

Comments